Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya (UNSMIL), umelaani mauaji ya kinyama ya wahamiaji 15 na wanaotafuta hifadhi” katika mji wa Sabratha (magharibi), nchini Libya, wakitaka uchunguzi ufanyike na wahusika wafikishwe mahakamani.
Miili 15 ya wahamiaji, baadhi yao walichomwa moto na iligunduliwa Oktoba 7, 2022 kwenye pwani ya Sabratha (kilomita 70 kutoka mji mkuu Tripoli), mahali ambapo ni sehemu ya kuondoka kwa maelfu ya watu wanaotafuta kila mwaka kufika pwani ya Italia.
Katika tukio hilo, Miili 11 iliyoungua ilipatikana ndani ya boti iliyoangaziwa na miili mingine minne ikiwa na majeraha ilipatikana nje, ingawa hali halisi bado haijabainishwa na mauaji hayo yanaaminika kutokea kutokana na mapigano ya silaha kati ya wasafirishaji haramu.
Umoja wa Mataifa UN, umeitaka Libya kufanya uchunguzi huru wenye uwazi ili haki itendeke huku ikisema, “Janga hilo ni ushahidi tosha kuwa upo ukosefu wa ulinzi kwa wahamiaji na wanaotafuta hifadhi nchini Libya na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu unaofanywa na biashara ya watu wenye nguvu na mitandao ya uhalifu.”
Kulingana na vyombo vya habari vya ndani, vimesema wahamiaji hao, wengi ni kutoka Afrika na Kusini mwa Jangwa la Sahara na waliuawa kwa kupigwa risasi kufuatia mzozo kati ya wasafirishaji haramu waliohusika katika mzozo huo kisha kuchoma moto mashua waliyokuwa wakisafiria.
Machafuko nchini humo, yalianza kufuatia kuanguka kwa utawala wa Muammar Gaddafi mwaka 2011, na yameifanya Libya kuwa njia inayopendelewa na makumi ya maelfu ya wahamiaji kutoka Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, nchi za Kiarabu na Asia Kusini, wenye shauku ya kufika Ulaya kupitia Italia.
Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM), imesema tangu mwanzoni mwa mwaka huu, wahamiaji 14,157 wamezuiliwa na kurejea Libya na watu 216 wamekufa wakijaribu kuvuka bahari ya Mediterania huku 724 wakiwa hawajulikani walipo na kudhaniwa kuwa wamekufa.