Wakati klabu ya Azam FC ikitajwa kuwa mbioni kuachana na wachezaji wao Mudathir Yahya na Salum Aboubakar ‘Sure Boy’ waliowasimamisha kwa utovu wa nidhamu, Maafande wa Jeshi la Polisi (Polisi Tanzania FC) wapo mbioni kusajili kupitia dirisha dogo.
Kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa Mudathir Yahya na Salum Aboubakar ‘Sure Boy’ wamekua nje ya kikosi cha Azam FC ambacho kinakabiliwa na Mshike Mshike wa Ligi Kuu Tanzania Bara, huku kikitolewa kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika.
Polisi Tanzania FC wanatajwa kuwa kwenye mipango ya kuwasajili wawili hao, ili kukiimarisha kikosi chao na kujiweka katika mazingira mazuri ya kuwania nafasi tatu za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu msimu huu 2021/22.
Hata hivyo Makamu Mwenyekiti wa Polisi Tanzania, Robert Munis alipoulizwa taarifa hizo alijibu: “Mbona safi tu, kama mwalimu akiwataka hao wachezaji sisi kama viongozi tutawasajili.”
“Hakuna timu ambayo haipendi kuwa na wachezaji wazuri kama hao, hususan Polisi Tanzania ambayo inataka kujiweka imara zaidi kwenye kuwania nafasi tatu za juu. Ila kwa sasa bado hakuna ripoti hiyo na timu inafanya vizuri.”
Polisi Tanzania FC imeshacheza michezo mitano ya Ligi Kuu, huku ikishika nafasi ya tatu katika msimamo kwa kufikisha alama 10, huku Azam FC ikiwa nafasi 8 kwa kumiliki alama 7.