Maafande wa Jeshi la Magereza Tanzania ‘Tanzania Prisons’ wamejipanga kurejesha Ubora wao katika Mshike Mshike wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kuanza vibaya msimu huu 2021/22.

Tanzania Prisons ilianza msimu huu kwa kusuasua, kwani hadi Ligi Kuu inasimama kupisha Michezo ya kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2022, Maafande hao walikua wameshacheza michezo mitano, wakipoteza michezo miwili na kuambulia sare katika michezo mitatu, matokeo ambayo yamewatupa kwenye nafasi ya mwisho kwenye msimamo wa Ligi hiyo.

Kocha msaidizi wa Tanzania Prisons, Shaban Kazumba amesema hawakuwa na mwanzo mzuri wa ligi na hicho kilichowakuta anaamini ni upepo ambao utapita.

“Matokeo ya michezo yetu ilizopita hayakuwa mazuri nadhani ni upepo tu, bado tuna matumaini tutarudi katika kasi yetu kama wachezaji watatuliza akili na kupambana kupata ushindi,” amesema Kazumba.

Kazumba alisema amewaeleza wachezaji umuhimu wa michezo ijayo ambapo wanatarajiwa kuwakaribisha Mbeya Kwanza Novemba 18, mwaka huu kwenye Uwanja wa Nelson Mandela mjini Sumbawanga mkoani Rukwa.

Amesema kulingana na mambo yalivyo, wakishinda mchezo mmoja wanaweza kutoka chini na kupanda nafasi za juu hivyo hawana wasiwasi.

Kocha huyo amesema mchezo huo ujao una umuhimu na wanajua Mbeya Kwanza siyo timu ya kubeza kwani imeanza ligi vizuri, hivyo wataingia kucheza kwa kujiamini lakini kwa tahadhari wakijua alama tatu zinahitajika.

“Mbeya Kwanza tulicheza nao mchezo wa kirafiki tukawafunga lakini hatuwabezi, hatuwezi kujua watakuja vipi, ni lazima tuwaheshimu,” amesema Kazumba

Prisons inaonekana kuwa na safu mbovu ya ulinzi na ushambuliaji wakifungwa jumla ya mabao sita na kufunga bao moja pekee katika michezo mitano.

Niyonzima aingia rekodi za FIFA
Rage aunyooshea kidole uongozi Simba SC