Kiungo Mkabaji wa Young Africans, Mudathiri Yahya amefunguka kuwa hawako tayari kuona wanapoteza kwa mara nyingi kwenye mchezo wao ujao dhidi ya Simba SC, kwani wanataka kurudisha heshima yao ndani ya timu hiyo.
Katika mchezo huo unatarajia kupigwa Jumapili (Novemba 05), mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam ambapo Simba SC watakuwa wenyeji.
Rekodi zinaonyesha kuwa Young Africans imepoteza mara mbili dhidi ya Simba SC, ikiwemo mchezo wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita 2022/23 na Ngao ya Jamii iliyofanyika Mkwakwani, Tanga.
Mudathiri amesema kuwa baada ya mchezo wao na Singida Fountain Gate FC, kocha wa timu hiyo, Miguel Gamondi alikuwa na kazi maalum ya kuyafanyia kazi madhaifu yao pamoja na ubora wa Simba SC.
Kiungo huyo amesema kuwa wanaenda kwenye mchezo mkubwa kwa sasa wapo bize na maandalizi ya mchezo huo kwa lengo la kupata matokeo ya ushindi kwa kuendelea kuongoza ligi hiyo.
“Maandalizi yako vizuri hatutakuwa tayari kuona tunaenda kupoteza huu mchezo kwa mara nyingi, tuko imara na mashabiki wajitokeze kusapoti timu iliendeleza ushindani.
“Jambo kubwa ni kuwa kila mchezaji hapa anatambua kuwa hautokuwa mchezo rahisi kwa sababu tunacheza na timu ambayo tunaifahamu vizuri na presha yake huwa ni kubwa kutokana na aina ya mchezo wenyewe, lakini matumaini yetu ni kuona tunashinda na kurudisha heshima yetu,” amesema Mudathir