Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe amechangia Umoja wa Afrika (AU) dola za kimarekani milioni 1 ($1m), baada ya kuuza mamia ya ng’ombe nchini kwake.
Kiongozi huyo amesema kuwa alitoa ng’ombe 300 lakini Wakulima wa Zimbabwe walimuunga mkono na kutoa mara mbili ya idadi hiyo, lengo likiwa kuisadia AU kuondokana na utegemezi wa nchi za Magharibi.
Mugabe alikabidhi hundi ya $1m kwa AU katika mkutano wa viongozi wa Umoja huo uliofanyika nchini Ethiopia, mwanzoni mwa wiki hii.
“Kama mkulina na Muafrika, kuchangia ng’ombe ni ishara ya mali, huja kiasilia tu,” alisema Mugabe mwenye umri wa miaka 93, wakati akiikabidhi hundi.
Suala la AU kujiwezesha kufanikisha shughuli zake yenyewe imekuwa agenda muhimu zaidi katika vikao vya hivi karibuni vya Umoja huo. Agenda hiyo ilianzishwa kwa nguvu katika mkutano wa 27 wa wakuu wa nchi wanachama uliofanyika jijini Kigali nchini Rwanda, mwaka mmoja uliopita.
Zimbabwe ambayo ilikuwa ikikabiliwa na tatizo la kiuchumi na upungufu wa chakula, mwaka huu umekuwa wa neema kwake kwani nchi hiyo inatarajia mavuno mazuri kulinganisha na miaka iliyopita.