Hospitali ya Taifa Muhimbili imeanza kusambaza mavazi maalumu (coverall) kwa kamati za dharura za Jiji la Dar es Salaam, ambayo ni sehemu ya mavazi ya watoa huduma (PPE) kuvaa ili kujikinga wakati wanatoa huduma kwa wagonjwa wenye maambuki mbalimbali ikiwemo Covid 19.
Akizungumza na wanahabari, Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Zuhura Mawona amesema kuwa baada ya kujadiliana na Serikali bei elekezi itakuwa Tshs. 50,000 kwa kila vazi moja.
Manispaa ya Kinondoni imenunua mavazi 15 yenye thamani ya Tshs. 750,000, Ilala mavazi 20 yenye thamani ya Tshs. 1,000,000 huku Manispaa nyingine zikiendelea kulipia ili kupata mavazi hayo.
“Kwa sasa tunaanza na vituo vilivyopo katika Manispaa za jiji la Dar es Salaam na mikoa mingine itafuata” amesema Mawona.
Amesema kuwa mahitaji ni makubwa katika mikoa mbalimbali hivyo kwa sasa Muhimbili imejikita katika kuongeza uzalishaji ili kukidhi mahitaji.