Nahodha wa klabu ya AS Vita Club Jeremie Mumbere ameipa nafasi klabu ya Simba SC kutinga nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika kwa kuitoa Kaizer Chiefs ya Afrika kusini.
Simba SC ilimfahamu mpinzani wake kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika hatua ya Robo Fainali, baada ya Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’ kuendesha Droo mwishoni mwa juma lililopita, mjini Cairo, Misri.
Mumbere ambaye aliyekua sehemu ya kiosi cha AS Vita Club wakati ikicheza dhidi ya Simba SC kwenye michezo ya hatua ya makundi, amesema wawaklishi hao wa Tanzania wapo vizuri, na wana uwezo mkubwa wa kuifunga Kaizer Chiefs kwenye michezo yote miwili (nyumbani na ugenini).
“Simba imeungana vizuri sana, wachezaji wao wanafurahia kuwa sehemu ya kikosi cha Simba, wanafurahia kucheza mpira, aina yao ya kucheza inavutia na ina watu wa kuwapatia matokeo hata katika mazingira magumu.”
“Kaizer Chiefs sio kwamba ni timu mbovu, hapana, ni timu nzuri ambayo ina kila kitu, wapo vizuri kiuchumi na wana wachezaji wenye majina makubwa na wakongwe lakini hawajakuwa na kipindi kizuri, matokeo yao yamekuwa ya kupanda na kushuka, ndio maana nawapa zaidi nafasi Simba ya kutinga nusu fainali kuliko wao.”
Simba SC ilitinga hatua ya Robo Fainali Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, kwa kuongoza kundi A, lililokuwa na timu za Al Ahly ya Misri, AS Vita Club ya DR Congo na Al Merreikh ya Sudan.