Baada ya mchakato mrefu kuhusu wapi Munir El Haddadi anastahili kucheza akiwa na timu ya taifa, hataimaye Shirikisho la Soka Duniani FIFA limempa ruhusa mchezaji huyo kuitumikia Morocco.
Kwa kipindi kirefu FIFA walikua wanasubiriwa kutoa tamko la wapi mchezaji huyo mwenye asili ya nchi za Morocco na Hispania, atakapocheza soka lake la kimataifa.
El Haddadi anaecheza nafasi ya kiungo wa pembeni wazazi wake wanatokea nchi za Hispania na Morocco, hali ambayo iliibua mkanganyiko wa wapi anastahili kucheza soka lake la kimataifa.
Mama mzazi wa mchezaji huyo wa zamani wa FC Barcelona ni raia wa Hispania huku baba mzazi akitokea nchini Morocco, lakini alianza maisha yake ya soka katika kituo cha kulea na kuendeleza vijana kwa vijana cha FC Barcelona ‘LA MASIA’.
Hata hivyo aliwahi kuzitumikia timu za vijana za mataifa hayo mawili, jambo lingine ambalo liliongeza mkanganyiko na kufikia hatua ya suala lake kufikishwa mbele ya FIFA.
Tangu mwaka 2017, El Haddadi amekuwa kwenye mchakato wa kupambana kubadilisha taifa la kuitumikia timu ya taifa kutoka Hispania kwenda Morocco.