Rais wa Uganda, Yoweri Museveni ametangaza hatua mpya za kudhibiti mienendo ya madereva wa malori yanayoingia nchini humo kutoka Mataifa jirani baada ya zaidi ya madereva 20 kupatikana na virusi vya Corona.
Amesisitiza kuwa kusitisha usafirishaji wa bidhaa itakuwa na athari kubwa lakini madereva hao ni tishio katika mapambano ya nchi hiyo dhidi ya corona huku akitoa mfano wa janga la UKIMWI kwa miaka ya 1980 na 1990 ambapo madereva wa malori walisambaza HIV kila walipopita.
Amesema hatua zaidi ni pamoja na kila lori kuwa na mtu mmoja yaani dereva pekee yake ambaye hataruhusiwa kulala hotelini wala nyumbani kwa watu akiwa Uganda na mienendo ya madereva hao itachunguzwa.
Mataifa ya Uganda na Kenya yamekuwa yakiwafanyia vipimo vya corona madereva wa malori katika mipaka yao hali iliyosababisha foleni ndefu ya magari hayo.