Rais wa Uganda, Yoweri Museveni amezitaka nchi za Magharibi kuhakikisha haziingilii siasa za nchi hiyo kwani ni mambo ya ndani ya nchi.
Museveni amezituhumu nchi za Magharibi ambazo hakuzitaja majina kuwa zinafanya njama ya kuingilia siasa za Uganda kwa kutoa misaada kwa vyama vya upinzani kupitia mgongo wa mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs).
“Ni muhimu kwa mataifa ya nje kukaa mbali na kutoingilia mambo ya ndani ya nchi ya nyingine,” Museveni alisema kwenye mkutano wake na vyombo vya habari Jumapili iliyopita.
“Kama kuna tatizo lolote ndani ya Uganda, nina uhakika nitalishughulikia vizuri zaidi ya watu wa mataifa mengine. NGOs ambazo zinafadhiliwa na nchi za kigeni hutoa fedha kwa wanasiasa wa upinzani, zinatoa ushauri na uongo kwa niaba yao,” aliongeza Rais Museveni.
Katika hatua nyingine, Museveni alisema kuwa Serikali yake imeongeza zaidi ya walinzi 1000 kwenye jiji la Kampala kwa lengo la kuimarisha ulinzi kufuatia matukio ya mauaji ya watu mashuhuri ikiwa ni pamoja na maafisa wawili wa polisi, mbunge na mwendesha mashtaka.
Ujumbe huo wa Rais Museveni umekuja ikiwa ni siku chache tangu mwanasheria wa Robert ‘Bobi Wine’ Kyagulanyi ambaye ni mbunge na mwanamuziki maarufu, kuitaka Marekani kusitisha misaada ya kijeshi kwa Uganda akidai kuwa misaada hiyo inatumiwa kuwatesa wananchi.
Bobi Wine ambaye yuko Marekani kwa ajili ya matibabu kutokana na kipigo alichopewa na askari wa kikosi cha jeshi kwa tuhuma za kusababisha vurugu na wafuasi wake kushambulia gari la msafara wa Rais, alikutana na mbunge wa Marekani katika juhudi za kutaka Serikali ya Donald Trump isiendelee kuisaidia Uganda kwa silaha za kijeshi.