Mshambuliaji kutoka nchini Zambia Kennedy Musonda amekiri kuridhishwa na sare ya 1-1, dhidi ya AS Real Bakamo iliyokua nyumbani jana Jumapili (Februari 26) ikicheza dhidi ya Young Africans, katika Uwanja wa Machi 26 mjini Bamako.
Young Africans ilicheza mchezo wake watatu wa Kundi D, Kombe la Shirikisho Barani Afrika, na kufanikiwa kukusanya alama nne zinazoendelea kuiweka nafasi ya pili katika msimamo wa Kundi hilo.
Mshambuliaji Musonda ambaye alisajiliwa Young Africans wakati wa Dirisha Dogo akitokea Power Dynamos ya nchini kwao Zambia, ametumia ukurasa wake wa Mtandao wa Instargram kuandika ujumbe uliothibitisha ameridhishwa na matokeo hayo.
Musonda ameandika: “Tulistahili alama tatu, lakini moja inatupa nguvu kupambana zaidi nyumbani.”
Katika mchezo huo uliochezeshwa na mwamuzi kutoka nchini Botswana Joshua Bando, Young Africans ilitangulia kupata bao kupitia kwa Mshambuliaji kutoka DR Congo Fiston Kalala Mayele dakika ya 60 kabla ya Kone hajafunga bao la kusawazisha dakika ya 90.
Young Africans itaendelea na Mbilinge Mbilinge za Kombe la Shirikisho Barani Afrika Jumatano (Machi 08) katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, kwa kuikaribisha AS Real Bamako.