Jeshi la polisi mkoa wa Tabora limemfikisha mahakamani muuguzi wa kituo cha afya cha cha kata ya Igurubi wilayani Igunga, Damian Mgaya kwa tuhuma za kumbaka msichana mwenye umri wa miaka 18 aliyefika kituoni hapo kwa lengo la kupata matibabu.
Kwa mujibu wa maelezo ya mwendesha mashtaka wa Jeshi la polisi katika Mahakama ya Wilaya ya Igunga, Elimajid Kweyamba, muuguzi huyo alimlewesha msichana huyo kwa dawa maalum za usingizi na kisha kumbaka akiwa usingizini.
Mwendesha mashtaka aliiambia mahakama hiyo kuwa Mgaya mwenye umri wa miaka 26 alitenda kosa hilo Julai 13 mwaka huu majira ya saa tano usiku.
- Video: Kesi CUF dhidi ya Bodi ya Wadhamini yazidi kuota mbawa
- Video: Mwanasheria wa Tundu Lissu agonga mwamba, ashindwa kuonana na mteja wake
Alifafanua kuwa kitendo cha kumpa msichana huyo dawa za usingizi bila sababu za kidaktari na pia kufanya ubakaji, ni makosa mawili ambayo yanatokana na vitendo hivyo vilivyo kinyume cha sheria ya adhabu.
Hata hivyo, mtuhumiwa alikana mashtaka hayo dhidi yake na alipewa dhamana baada ya kutimiza masharti ambayo ni kutoa kiasi cha shilingi milioni 2 na kuwa na mdhamini mmoja.
Kesi hiyo iliahirishwa hadi Agosti 1 mwaka huu.