Ujerumani leo inasherehekea miaka 30 ya kuungana tena kwa iliyokuwa Ujerumani Mashariki na Magharibi lakini hakutakuwa na shamrashamra kubwa kutokana na janga la virusi vya Corona.
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na rais wa shirikisho Frank-Walter Steinmeier wamehudhuria sherehe rasmi za siku ya muungano ambazo mwaka huu zinafanyika kwenye mji wa historia wa Potsdam, kilometa 25 kusini magharibi mwa mji mkuu, Berlin.
Kwa karibu mwezi mzima matukio kadhaa yamefanyika kuadhimisha miongo mitatu ya kuungana tena kwa Ujerumani mbili mnamo mwaka 1990, miezi michache tangu kuanguka kwa ukuta wa Berlin na kumalizika kwa enzi ya vita baridi.
Kiongozi wa uliokuwa muungano wa Kisovieti, Mikhail Gorbachev amesema sherehe za leo ni ishara kuwa migawanyiko barani Ulaya imedhibitiwa na kukumbusha kuwa mchakato wa kufikia hatua hiyo ulikuwa mgumu.