Na mwandishi wetu; Morogoro
Jumla ya watu 11 wamefariki dunia katika matukio mawili tofauti yaliyosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha mkoani Morogoro.
Katika tukio la kwanza Watu wanne wa familia moja wamefariki dunia baada ya kuangukiwa na ukuta wa nyumba wakati wamelala kutokana mvua iliyokuwa ikinyesha usiku wa mei 15, 2020.
Hayo yameelezwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro (SACP) Wilbroad Mutafungwa, ambapo amewataja watu hao kuwa ni Godfrey Agustin (35), Joyce Cloud (38), Mariana Godfrey (10) na Senorino Godfrey (5) Wote wakazi wa Konde na kwamba miili yao imeshafanyia uchunguzi na kukabidhiwa kwa
ndugu kwaajili ya taratibu za mazishi.
Katika tukio la pili lililotokea Mei 15, 2020 majira ya saa nane usiku katika kijiji cha Pemba Kata na Tarafa ya Mvomero Mkoani Morogoro ambapo watu 7 wakiwemo watoto 5 walifariki dunia kwa kusombwa na maji ya mvua Iliyonyesha maeneo ya milimani wakati wao wanaishi eneo la Tambarare.
Kamanda Mutafungwa Amewataja watu hao kuwa ni Peter Ferdnand (66), Tumbo John (37), Kauva Peter (35), Jack Tumbo (6), Kadudu Fikiri (9), Madi Fikiri (14) na Mtupe John (8) Wote wakazi wa kijiji cha
Pemba.
Inaelezwa katika tukio hilo pia mtoto mchanga wa kiume ambaye alikuwa hajapewa jina mtoto wa marehemu Kauva Peter, naye haonekani licha ya kuwa alikuwa amelala na familia yake ambapo inahisiwa kuwa naye amesombwa na maji na juhudi za kumtafuta bado zinaendelea.
Miili ya marehemu hao saba ambao wametambulika imeshafanyiwa uchunguzi na madaktari na kukabidhiwa kwa ndugu kwaajili ya taratibu za mazishi.
Jeshi la polisi limetoa pole kwa familia zote zilizokumbwa na maafa haya na kutoa wito kwa wakazi wote wanaoshi katika maeneo ya Tambarare kuchukua tahadhari hasa katika kipindi hiki ambacho mvua bado zinaendelea kunyesha, pia limetoa wito kwa watu ambao wanaishi katika nyumba ambazo si imara
kuchukua tahadhari zaidi ikiwemo kukagua nyumba zao mara kwa mara ili kuhakikisha usalama.