Kocha Mkuu wa Young Africans, Luc Eymael ametaja kikosi cha nyota ambao ataendelea kuwa nao msimu ujao huku akisubiri kuletewa nyota wapya aliowapendekeza.

Eymael amewataja Ditram Nchimbi na Morrison kuwa wachezaji muhimu sana katika mipango yake ya msimu ujao, wengine wakiwa ni walinda mlango Farouk Shikalo na Metacha Mnata; na mabeki Lamine Moro, Kelvin Yondani.

Viungo ni Said Juma Makapu, Feisal Salum ‘Fei Toto’, Papy Tshishimbi, Haruna Niyonzima na Mohammed Issa ‘Mo Banka’, huku kukiwa na maingizo mapya katika nafasi za mabeki wa pembeni na mawinga kutegemea na hali ya kiuchumi Jangwani itakavyoruhusu.

Lakini kama mambo yakienda ndivyo sivyo, mabeki wa pembeni watabaki wale wale, yaani Juma Abdul (kulia) na Japhary Mohammed (kushoto), huku mawinga wakiwa ni Mapinduzi Balama na Patrick Sibomana.

Hata hivyo, iwapo mambo yatakwenda kama yalivyopangwa kwa Wanajangwani hao kufanikiwa kusajili wachezaji wote waliopendekezwa, wapo watakaounda kikosi cha pili.

“Kama bajeti itaruhusu, nataka kuwa na vikosi viliwili vya nguvu ambavyo chochote kinaweza kucheza na kupata ushindi. Lengo letu ni lile lile kuwa msimu ujao Yanga iwe bingwa wa Tanzania,” Eymael amenukuliwa na gazeti la Bingwa.

“Nimekuta wachezaji wengi na wenye uwezo ndani ya timu, lakini kilichokuwa kinatukwamisha, baadhi yao hawakuwa na mazoezi ya kutosha na wengine kuwa na majeraha ya muda mrefu, ndio maana tumeshindwa kutoa upinzani katika ligi.

“Unakuta mchezaji ni mzuri na mashabiki wanamuamini sana, lakini ukimpanga tu anatoka na majeraha, hii inamaanisha kuna ambao wanatakiwa kufanyiwa tiba kabla ya kuanza msimu,” alisema.

“Kwa wachezaji niliowapendekeza, iwapo watasajiliwa wote hakuna timu itakayotuzuia kutwaa ubingwa msimu ujao.”

Eymael amesema atarejea nchini wakati wowote baada ya Serikali ya Ubelgiji kuruhusu safari za kutoka nje ya nchi hiyo kutegemea na maendeleo ya janga la virus vya Corona.

Mvua Morogoro: watu 11 wafariki dunia
Muuza duka afariki kwa ajali ya moto dukani