Mpango wa kusitishwa mapigano kwa siku nne kati ya Israel na Hamas, ili kuruhusu msaada kuingia Gaza na kuwachiwa mateka wanaoshikiliwa, unatarajiwa kuanza kutekelezwa kwa mara ya kwanza baada ya karibu wiki saba za vita huku Hamas wakisema mpango huo utaanza hii leo Alhamisi saa nne kamili asubuhi.
Hatua hiyo inaingia ukakasi baada ya Israel kusema mpango huo hautaanza leo na badala yake kudai huenda ikawa kesho Ijumaa ya Novemba 24, 2023 ambapo Mshauri wa usalama wa Taifa, Tzachi Hanegbi akisema wanaendeleaza mawasiliano kuhusu kuachiwa kwa mateka wao.
Aidha, Israel bado haijasema ni wakati gani itasitisha mashambulizi yake ya anga na ardhini katika eneo hilo la pwani na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, Waziri Benny Gantz na Waziri wa Ulinzi Yoav Gallant, wameapa kuwaleta nyumbani mateka wote na kuwaangamiza wanamgambo wa Hamas.
Kwa upande wake Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwashughulikia Watoto – UNICEF, ameuita Ukanda wa Gaza uliozingirwa kuwa ni sehemu hatari ya mtoto kuishi na kusema makubaliano yaliyofikiwa ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Hamas hayatoshi kuyaokoa maisha yao.