Serikali ya Kenya imetangaza tarehe ya kuzika mwili wa rais wa tatu wa Kenya Mwai Kibaki aliyeaga dunia Ijumaa, Aprili 22, 2022 ambapo atazikwa nyumbani kwake Othaya.
Akihutubia waandishi wa habari akiwa na familia ya Rais Kibaki, Waziri wa Usalama Fred Matiang’i amesema kuwa wameafikiana kuuzika mwili wa Hayati, Kibati siku ya Jumamosi, Aprili 30, 2022.
Matiang’i amesema, Ibada ya kitaifa itaandaliwa katika uwanja wa kitaifa wa Nyayo siku ya Ijumaa, Aprili 29, kabla ya mwili huo kusafirishwa hadi nyumbani kwake katika eneo bunge la Othaya kwa mazishi.
“Tumekamilisha mipango ya mwanzo ya mazishi ya kitaifa ya Rais Mstaafu Mwai Kibaki na tungetaka umma kujua kuwa haya yatafanyika Ijumaa, Aprili 29, katika uwanja wa kitaifa wa Nyayo Rais Kibaki kisha atalazwa Othaya siku ya Jumamosi, Aprili 30, 2022,” Waziri Matiang’i alisema.
“Mwili wa Rais Kibaki utakuwa katika Bunge la Kitaifa kwa siku tatu kati ya Jumatatu na Jumatano ili umma na viongozi wengine kutoa heshima zao za mwisho,” Matiang’i aliongeza.
Hayati Mwai Kibaki alishika nyadhifa mbalimbali katika huduma yake kwa taifa la Kenya na Wakenya na viongozi mbalimbali katika kumuomboleza Kibaki, wengi wakimtaja kama rais bora zaidi kuwahi kutokea nchini Kenya.
Kibaki aliwahi kuwa Mbunge Katika uchaguzi wa mwaka 1963, alishinda ubunge wa eneo la Donholm kwa sasa likifahamika kama eneo bunge la Makadara, mbunge wa Donholm hadi mwaka 1974 alipohamia kwao Othaya na kuchaguliwa katika kila uchaguzi hadi mwaka 2013 alipostaafu.
Kibaki pia aliwahi kuhudumu kama Waziri Baada ya kushinda ubunge wa Donholm mwaka 1963, na aliteuliwa kuwa Waziri Msaidizi wa Fedha na Mwenyekiti wa Tume ya Mipango ya Uchumi kabla ya kupandishwa mamlaka na kuwa Waziri wa Biashara na Viwanda mwaka 1966.
Kwa kuwa mfuasi mkuu wa KANU, Kibaki aliteuliwa Waziri wa Fedha na Mipango ya Uchumi mwaka 1969 na kushikilia nafasi hiyo hadi mwaka 1978 alipofariki Rais Jomo Kenyatta.
Mwai Kibaki alikua Makamu wa Rais Baada ya Makamu Rais Daniel Arap Moi kuchukua urais kufuatia kifo cha Rais Jomo Kenyatta, Kibaki aliteuliwa kuwa Makamu wa Rais na vilevile Waziri wa Fedha hadi mwaka 1982 alipoanza kukosana na Moi.
Kufuatia hilo Wizara ya Fedha ilitolewa kwake, akipewa Wizara ya Masuala ya Ndani lakini Mwaka 1988, alikosana zaidi na Rais Moi, akatemwa kama Makamu wa Rais na kupewa wadhifa wa Waziri wa Afya.
Aliondoka serikalini mwaka 1991 na kuunda chama cha Democratic Party (DP) baada ya kurejeshwa kwa mfumo wa siasa za vyama vingi, akijiandaa kwa uchaguzi wa 1992 ambao aligombea na kuibuka wa tatu.
Kiongozi wa Upinzani Katika uchaguzi wa mwaka 1997, Kibaki alimaliza katika nafasi ya pili na chama chake cha DP na kuwa kiongozi rasmi wa upinzani na kuwa Rais Katika uchaguzi wa mwaka 2002, aligombea urais na kumshinda mpinzani wake Uhuru Kenyatta.
Mwaka 2007, Kibaki alijihakikishia muhula wake wa pili kama Rais ila kwa njia ya kutatanisha na vurugu zilizojiri baada ya kutangazwa kwa matokeo kutia tope uongozi wake Alistaafu mwaka 2013 na kumpisha Uhuru Kenyatta.
Rais wa tatu wa Kenya Mwai Kibaki aliaga dunia mnamo Ijumaa, Aprili 22, 2022, akiwa na umri wa miaka tisini.