Scolastica Msewa – Dar es Salaam.
Serikali Nchini, imesema itaendelea kuipa umuhimu Sekta ya Madini ikiwemo kushirikiana na Wadau wa Madini katika kuendeleza mipango ya Taifa na kuibua fursa mbalimbali za kiuchumi zilizopo kwenye Sekta ya Madini nchini.
Hayo yamebainishwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipomwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar katika kufunga Mkutano wa Tano wa Kimataifa wa Madini na Uwekezaji wa mwaka 2023.
Amesema, Serikali ipo tayari na inaruhusu miradi ya maendeleo kutoka Sekta binafsi katika Utafutaji , Uchimbaji , uchorongaji na uongezaji thamani madini ili kufanikisha mikakati iliyopo kwa wachimbaji kwa wachimbaji wote nchini.
Majaliwa amefafanua kuwa Serikali ina Taasisi yake ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) ambazo zinafanya kazi ya utafiti , uchenjuaji na uchorongaji kwa kushirikiana na kampuni binafsi na kutoa wito kwa wadau wote walioshiriki katika mkutano huo kutumia hizo za ushirikiano wa kimkakati.
Aidha, ameongeza kuwa Serikali kupitia Taasisi ya GST ina mpango wa kufanya utafiti wa jiolojia kwa nchi nzima ifikapo mwaka 2030 ili kuwa na kanziData ya taarifa za jiolojia zitakazo tumika kuvutia wawekezaji wa madini ndani na nje ya nchi.
Kwa upande wake , Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesema Wizara imetumia Mkutano huo katika kukuza ushirikiano wa kikazi baina ya nchi na nchi kupitia mada mbalimbali zilizowasilishwa kama vile majadiliano kuhusu matumizi ya Nishati safi ili kupambana na Mabadiliko ya Tabia Nchi.
Mavunde ameongeza kwamba, sekta ya madini inaendelea kusimamia miradi mbalimbali nchini ambapo leo Oktoba 26 , 2023 kampuni ya Noble Helium imeanza kutafiti na kuchoronga Gesi ya Helium mkoani Rukwa.
Naye, Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Kheri Mahimbali amesema kwa katika Mwaka wa Fedha 2022/23 Wizara ya Madini ilikusanya Shilingi Bilioni 678.
Awali , Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Mathayo David Mathayo amesema kuwa kazi kubwa ya kamati ni kuishauri na kusimamia sekta ya madini ili ikamilishe malengo iliyojiwekea hivyo itaendelea kutoa ushirikiano mzuri kwa Sekta ya Madini.
Mkutano wa Madini na Uwekezaji Tanzania kwa mwaka 2023 umeongozwa na Kauli mbiu inayosema Uncloking Tanzania’s Future Mining Potential.