Mshambuliaji kutoka nchini Ghana Michael Sarpong ataendelea kuwa sehemu ya kikosi cha Young Africans, licha ya taarifa za kutemwa na klabu hiyo kusambaa kwenye mitandao ya kijamii.
Sarpong anahusishwa na taarifa za kuachwa na Young Africans, baada ya kusajiliwa kwa mshambuliaji kutoka nchini Burundi Fiston Abdoul Razak, ambaye alikamilisha mpango wa kujiunga na klabu hiyo kabla ya kufungwa kwa dirisha dogo la usajili mwishoni mwa juma lililopita.
Makamu Mwenyekiti wa Young Africans, Fredrick Mwakalebela, amesema taarifa za kuachwa kwa Sarpong sio za kweli, na bado wanaendelea kumtambua kama sehemu ya wachezaji wanaounda kikosi chao.
Amesema kuachana na mchezaji kama Sarpong kwa wakati huu sio jambo jepesi, hivyo watu wasifikirie kwamba nyota huyo ameachwa, kama taarifa zinavyoendelea kusambaa kwenye mitandao ya kijamii.
“Unafikiri kuachana na mchezaji ndani ya Young Africans ni kitu chepesi? Hilo halipo, kuna utaratibu ambao upo na kwa sasa mchezaji huyo bado ni mali ya Young Africans.” Amesema Mwakalebela.
Sarpong anadaiwa ameshaondoka nchini kuelekea China, kwa ajili ya kucheza soka la kulipwa.
Kuhusu tetesi hizo, Mwakelebela amesema mshambuliaji huyo huenda akaelekea China kufanya majaribio, na sio kuondoka moja kwa moja, kama inavyoelezwa.
Sarpong alisajiliwa Young Africans msimu huu akitokea nchini Rwanda baada ya kuachana na Rayon Sports, na mpaka sasa ameshaifungia klabu hiyo yenye maskani yake katika makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani mabao manne kati ya 29 katika michezo 18 ya Ligi Kuu Tanzania Bara.