Chama cha Ngumi za Kimataifa ‘BA’, kipo kwenye mazungumzo na moja ya mabondia kutoka katika mataifa matatu ya Afrika kwa ajili ya kuja nchini kuwania mkanda wao dhidi ya Hassan Mwakinyo katika pambano linalotarajiwa kupigwa Septemba 29, mwaka huu, jijini Dar es salaam.
Mwakinyo ambaye awali alitarajia kupanda ulingoni kuwania mkanda wa Dunia wa WBO kabla ya upepo kubadilika, sasa anatarajia kupanda ulingoni kuwania mkanda wa IBA baada ya pande hizo mbili kufikia makubaliano.
Akizungumza jijini Dar es salaam Promota wa pambano hilo kutoka PAF Promotion Company Limited, Ally Mndeme, amesema mpaka sasa mchakato wa kutafuta mpinzani wa Mwakinyo unaendelea vizuri kutoka katika mataifa matatu ya Afrika.
Amesema jukumu la kutafuta mpinzani wa Mwakinyo linashughulikiwa na chama husika cha kimataifa kwa ajili ya kumleta mtu ambaye anaweza kuleta upinzani kwa bondia huyo Mtanzania.
“Tumefikia hatua nzuri katika maandalizi ya awali kwa sababu sehemu kubwa ya hili pambano lipo kwenye kutafuta mpinzani mwenye vigezo vya kucheza na Mwakinyo.
“Jukumu lipo chini ya IBA wenyewe na mpaka sasa wametuambia wanawasiliana na mabondia kutoka katika mataifa matatu tofauti,” amesema Promota huyo.
Amesema hawajaelezwa ni mataifa yapi, lakini wanatarajia kupata mpinzani wake ndani ya Afrika na inaweza kuwa Afrika Kusini, Nigeria au Namibia.
“Katika mataifa hayo matatu mojawapo inawezekana na kama kutakuwa na mabadiliko mengine kuhusu mpinzani lazima watatuambia kwa sababu kwa upande wetu kama waandaji ni lazima tujulishwe, amesema Mndeme.