Jeshi la Polisi Mkoani Tanga linamshikilia Mwalimu wa Shule ya Sekondari Mkwakwani kwa kumpiga na kumsababishia madhara ya kiafya mwanafunzi, Suleiman Mohamed (18).
Mwanafunzi huyo inadaiwa alichapwa viboko juzi asubuhi na mwalimu huyo wa zamu aliyekuwa akiwaadhibu wanafunzi waliochelewa na waliokuwa wakipiga kelele darasani.
Aidha, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Benedict Wakulyamba amesema tayari mwalimu huyo yuko mikononi mwa Jeshi hilo na upelelezi wa suala hilo unaendelea.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Thobias Mwilapwa amewataka walimu kuwa waangalifu wakati wakiwaadhibu wanafunzi ili kukwepa madhara kwa wanafunzi.
“Tunalifuatilia kwa karibu tukio hili. Niseme kwamba tutachukua hatua stahiki ikithibitika kuwa umefanyika uzembe,” amesema Mwilapwa.
Hata hivyo, Baada ya kuchwapwa mwanafunzi huyo alikimbizwa katika Hospitali ya Rufani ya Bombo kwaajili ya matibabu ikielezwa kwamba tayari amepatiwa rufaa kuhamishiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya matibabu zaidi.