Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Kigoma, imeanza kusikiliza shauri la awali la makosa saba, likiwemo la kubaka mara sita na kumpa mimba mwanafunzi, yanayomkabili Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nyantore, Janson Rwekaza.
Akisomewa mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu mkazi Kigoma, Frola Mtarania, Mwendesha mashtaka wa Serikali Clement Masua, amesema kuwa mshtakiwa alikuwa na mahusiano na mwanafunzi ambaye kwasasa ana umri wa miaka 17 tangu mwezi Mei 2017, akiwa darasa la 5.
Aidha, katika makosa hayo Mwalimu Mkuu huyo anatuhumiwa kufanya mapenzi na mwanafunzi huyo mara 6, ikiwemo tarehe 7 na 6 na tarehe 16 mwezi wa nane, 2017, tarehe nyingine ni 10 Julai, 22 Agosti, 2018, pamoja na 3 Februari, 2019 na mwishowe kumpa mimba mwanafunzi huyo.
Mshtakiwa amekana mashtaka yote saba na yuko nje kwa dhamana huku shauri hilo likiahirishwa hadi Agosti 26, 2019.