Kocha Juma Mwambusi ametegua Kitendawili cha wapi alipo, baada ya Mashabiki wa Soka la Bongo kuhoji Swali hilo, kufuatia kutokuelekana kwake katika Benchi la Ufundi la Ihefu FC, wakati wa mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Young Africans.
Ihefu FC ilicheza ugenini juzi Jumatatu (Januari 17), Uwanja wa Benjamin Mpaka jijini Dar es salaam na kuambulia kisago cha 1-0.
Kocha Mwambusi amesema amejiweka kando kwenye kikosi hicho kwa ajili ya kushughulikia kwanza matatizo yaliyojitokeza ya kifamilia.
“Nimepumzika kidogo, nina majukumu mengine zaidi ya kuifundisha timu ya Ihefu, kwa muda huu sipo kwenye timu, kwa sasa ipo chini ya Zuberi Katwila ambaye yeye nimemkuta pale, nadhani kwa sasa wanaendelea vizuri kwenye mambo yao ya usajili kwa sababu mipango hiyo ilikuwa inaendelea.”
“Kuna mambo mengine yameingia kati hapa kwa hiyo nimeona kwanza niyashughulikie, akili yangu kwanza iwe kwenye hili jambo la kifamilia kwanza, nadhani baada ya kuweka sawa sawa nitakuwa na neno la kuzungumza kwa muda huu kwa kweli hakuna nitakachoelezea,” amesema Mwambusi.
Amekiri kuwa ni kweli hakuwepo kwenye kikosi tangu Januari 3 ambapo ilicheza mechi ya Ligi Kuu dhidi ya KMC na kushinda bao 1-0, huku akiongeza kuwa hana tatizo lolote lililomfanya aondoke na pia hakuna anachowadai.
“Mimi na Ihefu hakuna tatizo lolote, ndiyo maana hata wao wameruhusu nikashugulikie hayo matatizo kwa sababu wameona ni ya umuhimu vile vile, na hakuna ninachowadai,” ameongeza kocha huyo aliyetua kwenye klabu hiyo Septemba mwaka jana.