Kiungo Mshambuliaji wa Kagera Sugar Meshack Mwamita amejikuta akiwa njiapanda, baada ya kufikia kikomo kwa mkataba wake mwishoni mwa msimu huu 2022/23, huku Uongozi wa Klabu hiyo ukijipanga kufanya usajili wa haja sambamba na kuwasainisha mikataba mipya wachezaji watakaopendekezwa na Benchi la Ufundi.
Kagera Sugar inayonolewa na Mecky Maxime haikufanya usajili wowote wakati wa Dirisha dogo huku ikiwakosa baadhi ya nyota wake mwishoni mwa msimu akiwemo Abdulaziz Makame aliyevunjiwa mkataba na Anuary Jabir aliyekwenda kwenye majaribio nje ya nchi.
Mwamita alijiunga na Kagera Sugar msimu wa 2021/22 kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Gwambina baada ya kuifungia timu hiyo mabao tisa na msimu huu akiwa na Wanankurukumbi amefunga mabao manne na assisti tatu.
Winga huyo amefunguka baada ya kumaliza mkataba wake, huku kwa sasa akiwasikilizia mabosi wake na atawapa kipaumbele kama watakuwa tayari kufanya mazungumzo ya kuongeza mkataba mpya, lakini hatazifumbia macho ofa kutoka klabu nyingine.
“Namshukuru Mungu kwa kila jambo. Msimu huu haukuwa mbaya kwangu, nilianza kwa utofauti kidogo lakini baadaye nilibadilika na nikawa napafomu vyema na ndiyo maana nimekuwa nikitumika.”
“Malengo yangu binafsi sikuweza kuyafikia kwa sababu mbalimbali ambazo siwezi kuzitaja lakini najivunia kwa nilichokifanya kwani kimekuwa na msaada mkubwa katika timu yangu,” amesema Mwamita
Katibu wa timu hiyo, Ally Masoud alisema baada ya kutofanya usajili kwenye dirisha dogo safari hii wamejipanga kufanya usajili utakaoipa makali timu yao na kufanya vyema kwenye mashindano mbalimbali msimu ujao.