Shirikisho la Soka BArani Afrika ‘CAF’ limemteuwa Mwamuzi Abongile Tom wa Afrika Kusini kuchezesha mchezo wa Mkondo wa Pili wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika kati ya Simba SC dhidi ya Primero de Agosto.
Mchezo huo umepangwa kuunguruma Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam Jumapili (Oktoba 16) katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, kuanzia saa 10:00 jioni.
Abongile mwenye umri wa miaka 30, ndiye alichezesha mchezo wa Mkondo wa Pili wa Michuano hiyo msimu uliopita kati ya Simba SC dhidi ya Jwaneng Galaxy uliochezwa Oktoba 24, 2021, ambapo Mnayama alipoteza kwa mabao 3-1.
Matokeo hayo yaliifanya Simba itupwe nje ya mashindano hayo baada ya Jwaneng Galaxy kunufaika na kanuni ya bao la ugenini, kwani yalifanya matokeo ya jumla ya mechi mbili baina yao kuwa sare ya mabao 3-3 kufuatia Simba kushinda mabao 2-0 katika mchezo wa kwanza ugenini huko Botswana.
Simba inapaswa kuwa makini sana na Mwamuzi huyo kwani amekuwa na historia ya kumwaga kadi katika michezo anayochezesha.
Katika michezo mitatu ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo Mwamuzi huyo amechezesha, ametoa jumla ya kadi 16 ambapo kati ya hizo, nyekundu ni moja na kadi za njano ni 15.
Katika mchezo wa Jumapili (Oktoba 16), Abongile Tom atasaidiwa na Mwamuzi msaidizi namba moja Kgara Mokoena na Mwamuzi msaidizi namba mbili, Moeketsi Molelekoa na Mwamuzi wa akiba akipangwa kuwa Luxolo Badi wote wakitokea Afrika Kusini.
Kamishina wa mchezo huo atakuwa Lewis Blaze Madeleine kutoka Shelisheli huku Jean Claude Birumushahu kutoka Burundi akipangwa kuwa Mtathimini wa Marefa.
Daktari Limbanga Manfred Kinyero kutoka Tanzania ndiye atakuwa Ofisa wa kusimamia vipimo vya Uviko-19.