Mwamuzi Soka nchini Misri, Mohamed Farouk amefungiwa kwa muda usiojulikana na Chama cha soka cha nchi hiyo baada ya kukataa bao la Al-Nasr kwa kuangalia marudio ya bao hilo kupitia simu ya shabiki.
Refa huyo alikuwa akichezesha mchezo wa Ligi Daraja la Pili Misri kati ya Al-Nasr na Suez ambao ulichezwa mwishoni mwa juma lililopita.
Lakini kutokana na VAR kutokuwepo uwanjani mwamuzi huyo akachukua simu ya shabiki na kuangalia marudio ya bao la kusawazisha la Al Nasr na kulikataa na matokeo yakabaki 2-1.
Licha ya mashabiki wa Suez kumjia juu mwamuzi huyo baada ya Al-Nasr kusawazisha hapo ndipo akapewa simu ya shabiki mmoja aliyekuwepo jukwaani akaangilie marudio kabla ya kufungwa bao hilo.
Bao hilo ambalo mwanzoni lilitokana na mpira wa adhabu, mashabiki wa Suez waliiingia uwanjani kwa hasira, wakitaka bao hilo lisikubaliwe.
Kutokana na kitendo hicho mwamuzi huyo akakumbana na adhabu hiyo kali huku kiongozi wa Chama cha Marefa Misri (ERC), Victor Pereira akiunga mkono uamuzi huo.
Chama cha Marefa Misri kinasimamiwa na Pereira ambaye alichukua nafasi ya refa wa zamani wa Ligi Kuu England, Marc Clattenburg tangu Machi.
Baada ya Pereira kuunga mkono, kauli yake ikathibitishwa na chama cha soka cha Misri.
“Kamati itafanya uchunguzi kuhusu tukio hilo linalomkabili Farouk, refa wa mechi hiyo, kutumia simu kuangalia marudio ya tukio ni kosa”. Na kutokana na uamuzi huo inasemekana Farouk aliondoka uwanjani akisindikizwa na Jeshi la Polisi.