Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Wiliam Mkonda amethibitisha kutokea kwa kifo cha mwanafunzi wa Stashahada ya Uandishi wa Habari, Maria Basso (24).

Maria, ambaye alikua katika mwaka wa pili wa masomo Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma (SJMC), ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, amefariki dunia baada ya watu zaidi ya 10 kuvamia nyumbani kwao.

Amesema, tukio hilo lilitokea Septemba 14, 2022 majira ya saa 2:30 usiku eneo la Kawe mzimuni, ambapo kikundi cha wahalifu wakiwa na silaha za jadi, walivamia nyumbani kwa Paschal Basso (56).

Kamanda Mkonda ameongeza kuwa, baada ya watu hao kuvamia nyumba hiyo yenye vyumba 15, walivunja milango na kupora fedha, simu za mkononi, kujeruhi watu watatu na kumuua mtu mmoja, ambaye ni Maria.

Aidha amefafanua kuwa, “Tukio walilofanya wahalifu hawa ni baya na linalotakiwa kulaaniwa na kukemewa na Mtanzania yoyote anayechukia uhalifu kwa watu kama hawa ambao hawataki kutumia njia halali za kujitafutia kipato.”

Hata hivyo, Kamanda Mkonda amesema, “Tunaendelea kuwasisitiza viongozi wa serikali za mitaa na wananchi kwa ujumla kuimarisha vikundi vya ulinzi shirikishi katika kukabiliana na uhalifu wa aina hii katika maeneo yao.”

Bungeni: Spika aitaka Serikali kushughulikia uhalifu
Kenya: Naibu Gavana afariki akiwa ndani ya Ndege