Mwanajeshi wa zamani wa Chile, Patricio Ortiz Montenegro aliyetoroka jela yenye ulinzi mkali mwaka 1996 na kukimbilia uhamishoni, amerejea nchini humo na kupokelewa kwa heshima.
Montenegro alishiriki mapambano dhidi ya utawala wa kidikteta wa Jenerali Augusto Pinochet. Alikamatwa mwaka 1991 na kufungwa jela miaka 10 kwa kosa la kumuua askari polisi.
Lakini baada ya miaka mitano, alishirikiana na wafungwa wenzake watatu pamoja na mtandao wake kutoroka jela akiwa amewekwa kwenye ndoo kubwa na kisha kupokelewa na helikopta na kuelekea uhamishoni nchini Uswizi.
Desemba mwaka jana, Mahakama nchini Chile ilikubali maombi ya mwanasheria wake ya kufuta hati ya kukamatwa.
Jana, aliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Santiago ambako alipata mapokezi ya makumi ya watu wakiwa na bendera za chama cha Patriotic Front of Manuel Rodriguez (FPMR) ambacho alikuwa mfuasi wake.
“Nimefurahi sana kufika nyumbani, sikuwa nategemea kukaribishwa vizuri kama hivi. Nimereja kwenye nchi yangu baada ya miaka 23 kuungana na ndugu zangu,” BBC inamkariri.
Ripoti za Umoja wa Mataifa zinaeleza kuwa takribani watu 3,200 waliuawa na wengine 28,000 waliteswa vibaya katika kipindi cha utawala wa Jenerali Pinochet.