Mwanamke mmoja kutoka umoja wa falme za Kiarabu (UAE), alipata ajali ya gari mwaka 1991 na kupoteza fahamu lakini katika hali ya kustaajabisha ameamka kutoka kwenye koma baada ya miaka 27 akiwa amepona.
Munira Abdulla katika ajali alipata jeraha kwenye ubongo baada ya kugongwa na basi wakati akiwa ametoka kumchukua mtoto wake shuleni, wakati huo alikuwa na umri wa miaka 32.
Kwa upande wa mwanae Omar Webair yeye alikuwa na umri wa miaka minne wakati ajali hiyo inatokea ambapo yeye alikuwa amekaa katika kiti cha nyuma, hakujeruhiwa hata kidogo na alikutwa akiwa amekumbatiwa na mama yake.
Familia ya mwanamke huyo haikumkatia tamaa ya kumhudumia hadi mwaka jana alipoanza kupata nafuu kama mtoto wake anavyosema
“Sikuwahi kukata tamaa kwa sababu kila siku nilihisi kuwa kuna siku mama yangu ataweza kuamka” Omar ameeleza na kuongeza kuwa sababu kubwa iliyomfanya asimulie mkasa huu uliyomkuta mama yake nikutaka kuwaambia watu kuacha kukata tamaa kwa watu wanaowapenda na mtu akiwa koma haimaanishi amekufa.
“Mama yangu alikuwa amekaa na mimi katika kiti cha nyuma, na alipoona tunakaribia kupata ajali, alinikumbatia ili kuniokoa katika ajili hiyo”
Omar hakuumia bali alibaki na jeraha dogo kichwani na mama yake aliyeumia sehemu ya ubongo alichelewa kapata matibabu kwa saa kadhaa.
Alipokuwa akipatiwa matibabu alikuwa anakula kwa mrija na kumfanya aendelee kuishi na kwa mara kadhaa alifanyiwa mazoezi na vipimo vya viungo ili kuhakikisha kuwa misuli yake haidhoofiki kwa kuwa alikuwa hatembei.
Mwaka 2017, familia iliweza kupokea msaada wa fedha kutoka serikalini ili kumuwezesha Munira kwenda Ujerumani kwa ajili ya matibabu.
Alifanyiwa upasuaji kadhaa ili kurekebisha mkono wake uliopunguzwa na kuweka sawa misuli ya miguu, na kupewa dawa ili kuboresha hali yake ambazo zimemsaidia kuzinduka kwake.
Imekuwa ni kwa nadra sana watu kupona baada ya kupoteza fahamu (koma) kwa miaka mingi na kuendelea kuwa wazima kabisa, na mara nyingi tatizo hili huwapata wanao pata madhara katika Ubongo.