Watu wasiojulikana wanaodaiwa kuwa na silaha, wamemuua Mwanasiasa mashuhuri wa upinzani na mwanasheria wa haki za binadamu, Thulani Maseko akiwa nyumbani kwake nchini Eswatini.
Taarifa ya Msemaji wa Chama cha Upinzani, Sikelela Dlamini amesema Maseko aliuawa usiku kwa kupigwa risasi siku ya Jumamosi (Januari 21, 2023), huko Luhleko, umbali wa kilomita 50 kutoka mji mkuu wa nchi hiyo Mbabane.
Dlamini amesema, “ niliambiwa wauaji walimpiga risasi kupitia dirishani akiwa ndani ya nyumba na familia yake na tayari nimesikia tayari Serikali imetuma salamu za rambirambi kwa familia yake, ikisema kifo cha Maseko ni hasara kwa taifa.”
Maseko, alikuwa ni Mwanasheria Kiongozi wa Haki za Binadamu na Mwandishi wa maoni nchini humo, ambaye alikuwa na kesi inayoendelea Mahakamani dhidi ya uamuzi wa Mfalme Mswati juu ya kubadili jina la nchi toka Swaziland na kuipa jina la Eswatini kwa amri.