Mwandishi nguli wa nyimbo na mshindi wa tuzo ya Grammy, Norman Gimbel aliyefahamika zaidi kwa kuandika wimbo wa ‘Killing Me Softly’ amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 91.
Mtoto wake wa kiume, Tony Gimbel ameiambia The Hollywood Reporter kuwa baba yake alifariki Desemba 19 mwaka huu nyumbani kwake Montecito, California
Kampuni ya muziki ya BMI ya Marekani imeeleza kusikitishwa na kifo cha Gimbel ikimuelezea kuwa ni mwandishi aliyekuwa amebarikiwa kipaji cha aina yake na kwamba atakumbukwa na kiwanda cha muziki.
Mwandishi huyo wa mashairi ya nyimbo amewahi kuandika nyimbo kadhaa kubwa mbali na Killing Me Softly, ikiwa ni pamoja na The Girl from Ipanema.
Alizaliwa Brooklyn na kuanza kazi ya muziki akiwa na wafanyabiashara maarufu wa muziki David Blum na Edwin H Morris. Mafanikio yake ya awali yalikuwa ni pamoja na kuandika wimbo wa ‘Canadian Sunset’ ulioimbwa na Andy Williams mwaka 1956.
Mwaka 1973, alishinda tuzo ya Grammy kama mwandishi bora wa nyimbo. Amekuwa akiandika pia nyimbo maalum kwa ajili ya filamu kubwa kama Laverne & Shirley, Wonder Woman na HR Puffnstuff.