Mbunge wa Vunjo (NCCR-Mageuzi), ambaye pia ni Mwenyekiti mwenza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), James Mbatia amelazwa mara baada ya kupata ajali na kuvunjika mkono alipoteleza na kuanguka alipokuwa akishuka ngazi katika hoteli ya Uhuru iliyopo eneo la Shanty Town.
Mbatia amelazwa katika wodi za watu mashuhuri VIP, hospitali ya Rufaa ya KCMC mjini Moshi.
Taarifa hii imetolewa leo na msaidizi wa Mbatia, Hamis Hamis ambapo amesema tukio hilo limetokea jana mida ya saa 2:45 usiku wakati anaondoka hotelini hapo kurejea nyumbani.
“Bahati nzuri pale kulikuwa na daktari wa KCMC anaiwa Ansbert Sweetbert ndiye alitoa huduma ya kwanza hadi kumpeleka KCMC,” amesema Hamis.
Mbatia ametafutwa leo mchana amesema bado maumivu aliyonayo ni makali kutokana na kuvunjika mkono.
“Bado nina maumivu makali. Nashukuru sana Mungu na jopo la madaktari limeshakutana na watafanya uamuzi,” amesema.
Mbatia amesema alishapatiwa matibabu ya mwanzo baada ya vipimo vya X-Ray kuthibitisha amevunjika mkono, lakini madaktari wanafanya tathmini ni huduma gani zaidi apewe.