Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres ametuma salamu kwa Waislamu kote duniani akiwatakia kila la heri kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani akiwataka kutafakari na kujifunza suala la umoja na amani.
Katika ujumbe maalum kwa ajili ya mfungo huo, Guterres amesisitiza kwamba Ramadhani ni mwezi wa kutafakari na kujifunza na unawakilisha wakati wa kusanyika katika ulimwengu wa roho ya uelewa na huruma, iliyofungwa na vifungo vya ubinadamu wa pamoja.
Amesema, “Katika nyakati hizi ngumu, moyo wangu unajaa hisia za huruma na sala kwa ajili ya wale wanaopatwa na janga la migogoro, kulazimika kukimbia makwao na maumivu. Naongeza sauti yangu kwa wale wote wanaoadhimisha mwezi mtukufu wa Ramadhani, nikitoa wito wa amani, kuheshimiana na mshikamano.”
Hata hivyo, Guterres ametoa wito wa maadili ya mwezi huu uliobarikiwa, ili kujenga ulimwengu wa haki na usawa kwa wote ambapo mapema mwezi huu, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliitisha mkutano wa ngazi ya juu kuadhimisha kwa mara ya kwanza siku ya kimataifa ya kupinga chuki dhidi ya Uislamu.