Mbunge wa jimbo la Iramba, Mwigulu Nchemba amejibu tuhuma za Mbunge wa Kigoma mjini na kiongozi wa Chama cha Upinzani cha ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe mara baada ya kuuponda msaada uliotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli alioutoa kwa nchi za Malawi Msumbiji na Zambabwe kufuatia maafa waliopata kutokana na kimbunga cha Idai.
Zitto kupitia ukurasa wake wa Twitter amesema kitendo cha Serikali kugawa msaada kwa nchi hizo zilizokumbwa na mafuriko ni siasa na tambo.
Zitto ameongezea kuwa wakati wa uongozi wa Jakaya Mrisho Kikwete nchi hizo pia ziliwahi kupata maafa hayo na awamu hiyo zilitolewa tani zaidi ya 8000 za mahindi na hapakuwa na tambo zozote juu ya msaada huo uliotolewa.
Kupitia mtandao wa kijamii wa Instagram wa Mwigulu Nchemba amemjibu Zitto na kumwambia.
”Hii ni lugha ya mtu anayelilia ustaarabu pasipokuwa mstaarabu,” Msaada kufanyiwa siasa ? kwa utekelezaji mkubwa namna hii wa ilani ya uchaguzi ya CCM kwa jitihada za Rais Magufuli, Tufanyie siasa Msaada…Hakuna kijiji hakijaguswa, itakuwa umeme, maji, Barabara, elimu, bure, zahanati, kituo cha afya,, mawasiliano, msaada siasa, Usivyo na utu huoni utu unaona siasa, ”Watapiga kura hao waliopokea msaada huo”?. Ameandika Mwigulu.
Majibizano hayo ni kufuatia siku ya juzi rais Magufuli kutoa msaada kwa nchi ya Zimbabwe, Msumbiji na Malawi wa tani 200 za chakula pamoja na tani 24 za dawa kwa nchi hizo ambazo zimekumbwa na mafuriko ya kimbunga cha Idia.
Ambapo idadi ya watu 100,000 mpaka sasa wanahitaji kuokolewa kwa dharura katika Mji wa Beira nchini Msumbiji ambako zaidi ya kilomita 50 za ardhi zimefunikwa na maji baada ya kingo za mto Buzi kuvunjika.
Huku watu 300 wamefariki dunia kwa nchi za Msumbiji na Zimbabwe na Malawi wametangaza vifo vya watu 50.