Mwanachaama Mkereketwa wa Young Africans Mwigulu Nchemba ametamba kuwa, msimu ujao klabu yake itakua na kikosi imara.

Mwigulu ambaye pia ni Waziri wa Fedha na Mipango amesema uimara wa kikosi chao utatokana na maazimio ya wanachama ya kukubali kuingia kwenye mabadiliko kupitia Mkutano Mkuu uliofanyika jijini Dar es salaam mwishoni mwa mwezi Juni.

Amesema mabadiliko hayo ya kiutendaji yatakuwa na faida hadi kwenye maamuzi ya kufanya usajili wa nguvu, huku akiamini kikosi chao msimu ujao hakitashikika na yoyote katika michuano ya ndani na nje ya Tanzania.

“Kwanza timu hii ya Young Africans ni bora ndio maana unaona inaenda kushiriki mashindano hayo makubwa, lakini kubwa la kwanza ni hizo reform ambazo zinaenda kufanyika ili kuweza kuwa na kikosi imara zaidi”

“Ukitaka kujua kwamba hicho kikosi ni imara, unaweza ukaangalia timu ambayo iliifunga Al Ahly hapa, imepigwa goli dakika ya (11′) na haikufurukuta kabisa kuweza kurudisha”

“Kwa hiyo mabadiliko hayo yanayoenda kufanyika yanaendelea kuimarisha mpaka upande wa kikosi, naamini tutakuwa na kikosi bora cha kuweza kufanya vizuri kwenye mashindano makubwa”

“Tutafanya usajili wakutisha kujenga kikosi chetu…..Kusema wale jamaa [Simba] hawaishagi, kwa hiyo huwa tunawaacha waseme wee, sie tukienda Kigoma tunawanyamazisha” amesema Mwigulu Nchemba

Msimu huu 2020-21 Young Africans tayari imeshakosa taji la Ubingwa wa Ligi Kuu baada ya watani zao wa jadi Simba SC kulitetea kwa mara ya nne mfululizo.

Nafasi pekee iliyosalia kwa wanajangwani ni kuwania ubingwa wa Kombe la Shirikisho katika mchezo wa Fainali utakaowakutanisha dhidi ya Simba SC Julai 25, Uwanja wa Lake Tanganyika Mkoani Kigoma.

Hanspope: Waamuzi wa nchi hii ni 'UKAKASI'
Simba SC kukabidhiwa 'MWALI' Julai 18