Mwili wa aliyekuwa Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji, William Ole Nasha unatarajiwa kuagwa kesho Bungeni Jijini Dodoma na kisha kusafirishwa Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha kwa ajili ya mazishi siku ya Jumamosi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa mapema leo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Jenista Mhangama, mwili wa kiongozi huyo utaagwa kesho Bungeni saa 5 asubuhi kisha safari ya kuelekea Arusha itaanza.
“Kesho siku ya Alhamisi tutafanya buriani ya kitaifa itakayohusisha viongozi wote katika viwanja vya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania majira ya saa 5 asubuhi,kwa sasa tunaendelea na vikao vya ndani kati ya Ofisi ya Bunge na sehemu alikokuwa anaabudu marehemu kiimani ili kuona namna tutakavyompa heshima ya mwisho,”amesema Mhagama.
Aidha ameeleza kuwa baada ya mazungumzo yote Marehemu Ole Nasha atapewa heshima za mwisho kisha kuanza safari ya kuelekea kijijini kwake Arusha ambako atapumzishwa kwenye nyumba yake ya milele siku ya Jumamosi.
“Ijumaa na Jumamosi ndiyo siku ambazo zitakuwa za maziko kijijini kwake,hayo ndiyo maamuzi ya kikao chetu cha awali, tutakaa tena saa kumi jioni kuona kama kuna jambo lingine jipya tutawajulisha,kwa sasa ni hayo tu,”amesema Waziri Mhagama
Amesema Serikali kwa kushirikiana na familia ya marehemu Ole Nasha inaendelea kufanya mazungumzo pia na Chama Cha Mapinduzi ambacho ndicho kimemlea ili kufanikisha maandalizi yote muhimu kuanzia hatua za awali hadi mwisho wa maziko.
Katika hatua nyingine Waziri Mhagama amewashukuru watanzania kwa kuendelea kushirikiana na serikali katika kipindi hiki cha maombolezo huku akiwataka kuendelea kuwa watulivu.