Mshambuliaji Mohamed Mussa amekuwa mchezaji wa mwisho kusajiliwa Simba SC, katika kipindi cha Dirisha Dogo la Usajili, ambacho rasmi kilifungwa usiku wa kuamkia leo Jumatatu (Januari 15).
Simba SC imethibitisha kumsajili Mshambuliaji huyo wa zamani wa Gwambina FC na Mbeya City, leo Jumatatu majira ya saa nane Mchana, kwa saa za Afrika Mashariki.
Mohamed anajiunda na Simba SC akitokea Klabu ya Malindi SC ya Zanzibar, ambayo kwa mara ya mwisho alionekana akiitumikia, Wakati wa Michuano ya Kombe la Mapinduzi 2023.
Mshambuliaji huyo mwenye Umri wa Miaka 22, hadi anaondoka Malindi alikuwa amefunga Magoli saba kwenye Ligi Kuu ya Zanzibar, akishika nafasi ya pili kwenye Orodha Wafungaji Bora, nyuma ya Kinara,Yassin Mgaza mwenye Magoli nane.
Kwa Mantiki hiyo Simba SC imesajili wachezaji wanne kupitia Dirisha Dogo la Usajili 2022/23 ambao ni Saido Ntibazonkiza (Burundi), Ismail Sawadogo (Burkina Faso), Jean Baleke (DR Congo) na Mohamed Mussa (Tanzania).
Walioachwa Klabuni hapo kwa kutolewa kwa mkopo ni viungo kutoka nchini Nigeria Nelson Okwa na Victor Akpan waliotimkia Ihefu FC inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara.