Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi amevitaka Vikosi vya Ulinzi na Usalama kupanua wigo katika shughuli za kilimo cha miwa, ili kukiwezesha kiwanda cha Sukari Mahonda kuwa na malighafi ya kutosha.
 
Mwinyi amesema hayo Mahonda Mkoa wa Kaskazini Unguja, wakati alipokitemebela Kiwanda hicho na kuangalia mchakato mzima wa uzalishaji wa sukari pamoja na kuzungumza na Uongozi,  wafanyakazi, wawakilishi wa wakulima wa nje pamoja na Wawakilishi wa Vikosi vya SMZ.
 
Amevitaka vikosi vya Ulinzi na Usalama, ikiwemo Mafunzo, JKU na KVZ kupitia nguvu kazi waliyonayo, zana za kilimo pamoja na ardhi ya kutosha iliyopo kuongeza juhudi na kuongeza uzalishaji wa miwa katika maeneo yao.

Mwinyi amesema hali ya kilimo hicho ilivyo hivi sasa katika Vikosi hivyo haiendani na uwezo halisi wa vikosi, hivyo akawataka kuongeza uzalishaji kwa kigezo kuwa kutawaongezea kiwango cha  mapato.
 
Ameeleza kuwa Serikali itazipatia ufumbuzi changamoto mbali mbali zinazokikabili Kiwanda hicho, huku akiutaka uongozi wa kiwanda  kuyatatua matatizo ya wafanyakazi mapema iwezekanavyo.
 
Aidha, amesema pamoja na mambo mengine Serikali itaangalia bei ya sukari, pamoja na upatikanaji wa ardhi bora kwa ajili ya kilimo cha miwa sambamba na kuitaka Wizara ya Kilimo , Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo kuwawezesha wakulima wa kilimo cha miwa kutumia njia ya umwagiliaji ili kiwanda hicho kiweze kupata malighafi zaidi.

Habari kubwa kwenye magazeti leo, Machi 8, 2021
Mkurugenzi, mkewe waliokufa maji Dodoma kuzikwa Iringa