Naibu Waziri wa TAMISEMI David Silinde amemsimamisha kazi Mwalimu Shela Mwangoka wa shule ya sekondari ya Momba katika wilaya ya Momba Mkoa wa Songwe kwa kudaiwa kutoa lugha ya dhihaka kwa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan katika kadamnasi ya watu.
Hayo yamebainika baada ya Emily Skanyika na Jacob Miyala kutoa kero kwa Katibu wa Itikakadi na Uenezi Taifa wa CCm, Shaka Hamduni Shaka, kwenye mkutano wa shina kati ya wananchi wa kijiji cha Washo kata ya Myunga Wilaya ya Momba, kuhusiana na matumizi mabaya ya lugha ambayo mwalimu huyo amekuwa akiitumia mara kwa mara.
Aidha Naibu Waziri Silinde amesema kuwa amefanya uchunguzi mdogo baada ya kusikia malalamiko hayo kujiridhisha na kugundua kua ni tabia ya Mwalimu huyo kufanya hivyo, na mara ya mwisho ni hata wiki moja aijapita akiwa sokoni alipoona Rais Samia kaongeza madaraja na mishahara kwa watumishi wa umma akasema ni hongo ili amuunge mkono akasema awezi muunga mkono sababu ni mwanamke.
“Hatuko tayari kufanya kazi na watu ambao hawaheshimu mamlaka,nimemuagiza afisa elimu wa wilaya ya Momba huyu mwalimu anasimamishwa kazi kuanzia leo na baada ya hapo hatua nyingine za kinidhaamu zitafuata ikiwemo jambo lake kupelekwa katika tume utumishi ya walimu,” Amesema Naibu waziri Silinde.
Kwa upande wake Katibu wa Itikadi na Uenezi Taifa CCM Shaka Hamdu amewaonyo watumishi wa umma wenye tabia kama za Mwalimu Shela kuacha mara moja vinginevyo atachukuliwa hatua kali za kinidhamu.