Wachezaji Sadio Kanoute, Israh Mwenda, Jimmyson Mwanuke na Mzamiru Yassin hawatakuwa sehemu ya kikosi cha Simba SC kesho Alhamis (Oktoba 27), kitakachoikabili Azam FC katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Simba SC itakua Mgeni kwenye mchezo huo, ambao awali ulipangwa kuchezwa Uwanja wa Azam Complex, Chamazi lakini Uongozi wa Azam FC ulitangaza maamuzi ya kuuhamisha Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Kaimu Kocha Mkuu wa Simba SC Juma Mgunda, amethibitisha atawakosa wachezaji hao alipozungumza na Waandishi wa Habari leo Jumatano (Oktoba 26) majira ya Mchana, kuhusu maandalizi ya kikosi chake kuelekea mchezo huo.
Amesema Wachezaji Sadio Kanoute, Israh Mwenda na Jimmyson wote wanasumbuliwa na maradhi, tofauti na Mzamiru ambaye anatumikia adhabu ya kukosa mchezo moja, kufuatia kufikisha idadi ya kadi tatu za Njano.
“Kikosi changu kipo sawa kabisa kuikabili Azam FC, kwa bahati mbaya nitaendelea kumkosa Sadio Kanoute na Jimmyson ambao walikosekana kwenye mchezo wetu dhidi ya Young Africans, na sasa wanaungana na Israh Mwenda aliyeumia Jumapili.”
“Mzamiru ataukosa mchezo wetu wa kesho kutokana na kanuni za bodi ya Ligi ‘TPLB’ kwa sababu mchezaji aliyepata kadi tatu za njano haruhusiwi kucheza mchezo unaofuata, ndivyo ilivyo kwa Mzamiru, kwa hiyo kesho atakosekana.”
“Kesho tunaenda kucheza na Azam FC, tunawaheshimu Wachezaji wa Azam FC na walimu wao. Mechi ya Derby imeshaisha na sisi tulikiwa tunajua baada ya Derby tutacheza na Azam FC, hivyo tayari tulishafanya maandalizi yake.” amesema Kocha Mgunda
Simba SC yenye alama 14 inakwenda kukutana na Azam FC ikiwa na deni la kurejea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya kushushwa na Mtibwa Sugar iliyofikisha alama 15, kufuatia ushindi wa 1-0 dhidi ya Dodoma Jiji FC jana Jumanne (Oktona 25).
Azam FC wao wataingia Uwanjani wakiwa na kumbukumbu mbaya ya kupoteza mchezo uliopita dhidi ya KMC FC iliyowachabanga mabao 2-1, siku ya Ijumaa (Oktoba 21), Uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam.