Mwanachama wa Young Africans Haji Omari Shamte ‘Mzee Mpili’ amesema ana uhakika Simba SC watapoteza tena mchezo dhidi ya klabu yake, kwenye mchezo wa Fainali ya Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ utakaochezwa mjini Kigoma, Uwanja wa Lake Tanganyika.

Mzee Mpili ametoa tambo hizo alipozungumza kwenye kipindi cha Kideo Soka kilichorushwa jana Jumatatu (Julai 05) na Dar24 Media #taarifabilamipaka akiwa sambamba na mashabiki wa klabu za Simba na Young Africans maeneo ya Karume jijini Dar es salaam.

Amesema ushindi wa siku Jumamosi (Julai 3), yeye alikuwa ni mchezaji namba moja kwa kuwa ana watu, hivyo hana mashaka na mchezo wa Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ utakaochezwa Julai 25, huku akimsisitiza kwamba lazima alipwe fedha ambayo aliahidiwa na Manara ambayo ni milioni moja.

“Mimi ninasema kwamba mchezo wetu ule pale taifa nilikuwa mchezaji namba moja na kuelekea kwenye mchezo wetu Kigoma nina amini kwamba nitaucheza na tutashinda.

“Siwezi kushindana na Manara, yeye ni mtoto mdogo haniwezi na mimi nina watu wakubwa kila mahali, sasa ninasema hivi kwa kuwa aliniahidi atanipa milioni moja ninaitaka.

“Yeye mwenyewe Manara alisema kuwa ohh Mzee Mpili ukitufunga sisi nitakupa milioni moja, basi sikumuomba mwenyewe amesema naitaka milioni moja yangu na ninasema kwamba Kigoma tunashinda tena,” alisema Mzee Mpili

Ushindi wa Young Africans dhidi ya Simba SC, umeifanya klabu hiyo kufikisha alama 70, ambazo zinaendelea kuwaweka kwenye mbio za kuwania ubingwa wa Tanzania Bara msimu huu 2020/21.

Simba SC wanaendelea kuwa na alama 73, zinazowaweka kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, huku ikisaliwa na michezo minne dhidi ya KMC FC, Coastal Union, Azam FC na Namungo FC.

Ndalichako atoa wito kwa wabunifu
Mauya: Lile goli sikupanga, ilitokea tu!