Waandamanaji wamefurika leo katika mitaa ya jiji la Harare nchini Zimbabwe wakichoma matairi na kuharibu baadhi ya miundombinu, wakipinga tangazo la Serikali la kupandisha bei ya mafuta.
Maandamano hayo ya wananchi wenye hasira, yameshuhudiwa ikiwa ni siku mbili tangu Rais Emmerson Mnangagwa atangaze kupanda kwa bei ya mafuta kwa 150% ikiwa ni jitihada za kupambana na anguko la uchumi.
Wakaazi wa mji wa Epworth ulioko Kilometa 36 kutoka Harare walijiunga katika maandamano ya siku tatu yaliyoitishwa na chama cha wafanyakazi wa eneo hilo kuanzia leo.
“Barabara kuu ya mji ilifungwa kwa kutumia mawe na waandamanaji, hakuna usafiri wa abiria na magari yote ya abiria yamezuiwa kubeba watu,” Reuters imemkariri Phibeon Machona, mkaazi wa Epworth.
Aidha, imeripotiwa kuwa Polisi wamefyatua mabomu ya machozi kuwatawanya waandamanaji katika jiji la Bulawayo, waliokuwa nje ya Mahakama ya Kuu ya nchi hiyo.
Ukosefu wa fedha kwa wananchi wengi nchini humo unazidi kuongezeka, hali inayotishia utulivu uliokuwepo tangu Robert Mugabe ajiuzulu nafasi ya Urais kutokana na maandamano yaliyoungwa mkono na Jeshi la nchi hiyo.
Serikali ya Zimbabwe ilitangaza kupanda kwa bei ya mafuta kupitia kwa Mamlaka ya Usimamia wa Nishati, hali iliyoashiria kuongezeka kwa gharama za maisha kwa wananchi ndani ya nchi hiyo ambayo kiwango cha ukosefu wa ajira ni 80%.
Rais Mnangagwa anakabiliwa na changamoto ya kuzishawishi nchi zenye nguvu kiuchumi kuondoa vikwazo vyote vilivyowekwa wakati wa utawalawa Mugabe.
Mtihani huu wa maandamano ya kupinga hali ya uchumi ni wa kwanza kwa Mnangagwa, lakini unafanana na hali ilivyoanza kuwa hususan katika miaka mitatu ya mwisho ya Mugabe.