Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans Nasreddin Nabi amesema kikosi chake kitapaswa kuwa na mabadiliko ya kiuchezaji ili kufanikisha mpango wa kufuzu hatua ya Makundi Kombe la Shirikisho Barani Afrika.

Young Africans itacheza mchezo wa Mkondo wa Kwanza dhidi ya Club Africain ya Tunisia keshokutwa Jumatano (Novemba 02), katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, kisha itakwenda mjini Tunis-Tunisia kucheza mchezo wa Mkondo wa Pili Novemba 09.

Kocha Nabi amesema kikosi chake kitakua na mtihani wa kupambana na timu yenye utamaduni wa soka la Tunisia, hivyo hana budi kubadili mfumo wa uchezaji kwenye mchezo huo, ambao unasubiriwa kwa hamu kubwa na Mashabiki wa soka nchini Tanzania.

Amesema mchezo huo utakua mgumu kutokanana kila upande kuhitaji kuvuka Hatua hii ya mtoano na kutinga Hatua ya Makundi, huku Club Africain ikitegemea sana mchezo wa Mkondo wa Pili ambao utachezwa kwao ili kujua hatma yao ya kufuzu.

“Hii ni mechi ngumu (dhidi ya Club Africain), tunakwenda kukutana na timu ambayo inacheza kwa utamaduni wa Watunisia, kupambana sana kwa nguvu, hii ni lazima tuwe na mabadiliko makubwa katika nidhamu ya ukabaji na kuzuia kwenye eneo letu la ulinzi.

“Najua tunaweza kushinda kwa kuwa tuna ubora wa kutengeneza nafasi na hata kuzitumia, kule mbele tunatakiwa kucheza kwa faida ya timu maombi yangu na nitazungumza sana na wachezaji juu ya umuhimu wa nidhamu ya wakati tumepoteza mpira na wakati tunao,”

“Ni kweli tunahitaji kufanya kazi kubwa katika eneo la ulinzi, nafurahi kuona Bacca (Ibrahim) anakuja vizuri kwa kupata nafasi kikosini, atatuongezea kitu zaidi, lakini kwanza ni kufuta makosa na kushambulia zaidi” amesema Nabi

Young Africans iliangukia Hatua ya Mtoano Kombe la Shirikisho Barani Afrika, baada ya kutolewa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika kwa kufungwa na Al Hilal jumla ya mabao 2-1.

Kwa upande wa Club Africain ambayo tayari imeshawasili jijini Dar es salaam, ilitinga hatua ya Mtoano Kombe la Shirikisho baada ya kuibamiza Kipanga FC ya Zanzibar mabao 7-0.

Bacca anogewa na mziki wa Young Africans
Sheikh aomba msaada wa dharula vifo vya watu 100