Kocha Mkuu wa Young Africans Nasreddine Nabi, ameonesha matumaini ya kuibuka na ushindi kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba SC, utakaochezwa Jumamosi (Septamba 25) Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Nabi ametoa tambo hizo, baada ya kurejea Dar es salaam akitokea Port Harcout, Nigeria alipokua na kazi kubwa ya kupambana na Rivers United katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika hatua ya awali.
Kocha huyo kutoka nchini Tunisia amesema mchezo dhidi ya Simba utakua na ushindani mkubwa, lakini anaamini kikosi chake kitafanya vizuri, kutokana na uwepo wa wachezaji wenye uzoefu ambao hakuwatumia kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.
“Kuhusu mchezo wa Jumamosi, utakua mgumu lakini nitajiandaa kikamilifu ili kufanikisha lengo la ushindi ambao utarejesha amani kwa mashabiki wetu,”
“Siku hiyo itakuwa tofauti kwa kuwa nitakuwa na maingizo mengine kama Djuma Shabani, Mayele Fiston, ambao wanaruhusiwa kucheza mechi hiyo, hivyo wataongeza nguvu katika kikosi,” amesema kocha Nabi.
Ikumbukwe kuwa mchezo wa Ngao ya Jamii huzikutanisha timu zilizotwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara na Kombe la Shirikisho (ASFC), lakini kwa msimu huu imekua tofauti kwani Simba SC ndio Bingwa wa michuano yote hiyo.
Kanuni ya mshindi wa pili wa Ligi Kuu ambaye ni Young Africans kucheza mchezo huo wa Ngao ya Jamii imetumika, na sasa watani wa jadi watakutana kwa mara ya nne mfululizo mwaka huu 2021.