Licha ya kukabiliwa na mchezo wa hatua ya pili ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya Pyramids ya Misri, Benchi la ufundi la Azam FC, limeuweka kiporo mchezo huo na kugeukia Ligi Kuu Tanzania Bara msimu 2021/21, ambao utaanza rasmi juma lijalo.

Azam FC ilivuka hatua ya awali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika kwa kuifunga Horseed FC ya Somalia jumla ya mabao 4-1, Uwanja wa Azam Complex Chamazi jijini Dar es salaam.

Kocha Msaidizi wa Azam FC, Vivier Bahati, amesema baada ya kumaliza mtohani wa mchezo huo wa kwanza wa kimataifa, akili na nguvu zao sasa ni kwenye michezo mitatu ya ligi kabla ya kukutana na Pyramids michuano hiyo ya CAF.

Amesema kwa sasa wanaangalia michezo ya ligi itakayowakabili wakianza dhidi ya Coastal Union mchezo utakaochezwa Septemba 27, mwaka huu na baada ya hapo wataenda Kilimanjaro kuwavaa Polisi Tanzania na kisha kurudi Dar es Salaam kumalizina na Young Africans.

“Tunahitaji kufanya vizuri msimu huu wa ligi, tupambane kupata pointi zote tisa na baada ya mechi hizo, tutakuwa tumeimarika zaidi na kuanza kufikiri mchezo wetu wa kimataifa dhidi ya Pyramids,” amesema Bahati

Amesema msimu huu malengo yao makubwa ni kuhakikisha wanafanya vizuri zaidi katika Ligi Kuu kwa kuvuna pointi muhimu katika kila mechi pamoja na kufanya vizuri michuano ya kimataifa kwa kusonga mbele hadi kucheza hatua ya makundi.

“Mechi za ligi zitatusaidia kuimarika na kuwa bora zaidi kukutana na wapinzani wetu Pyramids, timu yenye uzoefu mkubwa wa michuano hii ya kimataifa na tunahitaji kufanya vizuri kufikia malengo yetu,” amesema kocha huyo.

Msimu uliopita Azam FC ilimaliza katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania bara, ikitanguliwa na young Africans na Simba SC iliyotawazwa kuwa Mabingwa mara nne mfululizo.

Nabi atamba kuichapa Simba SC Jumamosi
Kocha Gomes ashusha pumzi Simba SC