Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) Athumani Amasi amewataka wasimamizi, wamiliki wa shule, walimu, wazazi na walezi kutojihusisha kwa namna yoyote na vitendo vya udanganyifu kwenye mitihani ya kidato cha nne iliyoanza leo nchini.
Ametoa Onyo hilo wakati akizungumza na waandishi wa habari amesema kuwa yeyote atakayejihusisha na udanganyifu hatabaki salama, ameeleza kuwa mtihani huo na wa maarifa (QT) utafanyika hadi Desemba Mosi mwaka huu katika shule za sekondari 5,212 na vituo vya watahiniwa wa kujitegemea 1,794 na maandalizi yote wa mithani huo yamekamilika.
“Wadau wote wanaombwa kutoa taarifa katika vyombo husika wanapobaini mtu au kikundi cha watu kujihusisha na udanganyifu wa mitihani wa aina yoyote, pia Baraza linawataka wamiliki wa shule kutambua kuwa shule zao ni vituo maalumu vya mitihani, hivyo hawatakiwi kwa namna yoyote kuingilia majukumu ya wasimamizi wa mitihani,”amesema Amasi
Amasi aliagiza kamati za mitihani za mikoa, halmashauri, manispaa, jiji na miji zihakikishe taratibu za uendeshaji wa mitihani ya kitaifa zinazingatiwa ukiwamo usalama na utulivu wa mazingira ya vituo vya mitihani na zizuie mianya ya udanganyifu.
Aidha, amesema watahiniwa 566,840 wamesajiliwa kufanya mtihani wa kidato cha nne mwaka huu na kati yao watahiniwa wa shule ni 535,001 na watahiniwa wa kujitegemea ni 31,839.
Aidha amesema, kati ya watahaniwa 535,001 wa shule waliosajiliwa, wavulana ni 247,131 sawa na asilimia 46.19 na wasichana ni 287,870 sawa na asilimia 53.81 wakati watahiniwa wenye mahitaji maalumu jumla yao ni 852 ambapo kati yao wenye uoni hafifu ni 480, wasioona 62, wenye ulemavu wa kusikia 19, wenye mtindio wa akili 152 na wenye ulemavu wa viungo vya mwili ni 139.
Alisema kwa mwaka huu kuna ongezeko la watahiniwa 28,816 sawa na asilimia 5.36 ikilinganishwa na watahiniwa 538,024 waliosajiliwa mwaka jana.
Pia amesema, watahiniwa wa kujitegemea 31,839 walisajiliwa na miongoni mwao wavulana ni 13,556 sawa na asilimia 42.58, wasichana 18,283 sawa na asilimia 57.42 na watahiniwa wa kujitegemea wenye mahitaji maalumu ni 13 ambapo wenye uoni hafifu ni wawili na wasioona 11.
“Jumla ya watahaniwa 12,090 wamesajiliwa kufanya mtihani wa maarifa ambapo wanaume ni 4,096 sawa na asilimia 33.88, wanawake ni 7,994 sawa na asilimia 66.12 na watahiniwa wa maarifa wenye mahitaji maalumu wapo 36 wote ni wenye uoni hafifu,”amesema Amasi.