Klabu ya Simba SC na Young Africans zimeombwa kupambana vilivyo ili zifanye vizuri katika hatua ya Makundi ya Michuano ya Kimataifa inayoratibiwa na Shirikisho la Kandanda Barani Afrika ‘CAF’.

Simba SC itacheza hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, huku Young Africans ikifuzu hatua ya Makundi Kombe la Shirikisho Barani humo, kwa kuifunga Club Africain bao 1-0 nyumbani kwao Tunis-Tunisia juma lililopita.

Ombi hilo kwa Simba SC na Young Africans limetolewa na Rais wa TFF Wallace Karia alipohutubia katika Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania unaofanyika jijini Mwanza.

Awali Rais Karia alizipongeza Klabu hiyo kwa kufanya vizuri na kutinga hatua ya makundi ya michuano hiyo huku akizitaka kujiandaa vyema na kufika hatua kubwa ikiwamo Nusu Fainali na Fainali.

“Tanzania sasa hivi tuko vizuri kwenye mpira wa miguu tumeheshimisha Kanda yetu ya CECAFA na kwenye uwakilishi wa klabu timu zetu zimekuwa zikifanya vizuri, katika Afrika ni nchi 12 zinazowakilishwa na timu nne na tumefanya hivyo kwa miaka mitatu, ni dhamira yangu kuhakikisha nafasi hiyo hatuiachii,”

“Ni matumaini yangu Young Africans na Simba SC hawatatuangusha watafanya vizuri makudi na kutupa hizo pointi 10 zinazohitajika,” amesema Karia.

Katika hatua nyingine Rais Karia ameipongeza timu ya Simba Queens kwa kufika Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa wanawake, huku akitamba kuwa alitamani timu hiyo ifike Fainali na kubeba ubingwa ili mwakani Tanzania iwakilishwe na timu mbili ambapo amewaomba wadau kuwekeza kwenye soka la wanawake kwani linapiga hatua kwa haraka.

Rais huyo akiwahutubia wajumbe na wageni waliohudhuria mkutano huo amesema huu ni mwaka wa mafanikio kwa Tanzania ambapo imepata mafanikio mbalimbali ikiwamo timu ya taifa ya wanawake chini ya umri wa miaka 17 (Serengeti Girls) kufuzu kwa mara ya kwanza kombe la Dunia na kufika robo fainali.

Amesema Mpango mkakati wa Shirikisho hilo wa mwaka 2018-2024 moja ya malengo ilikuwa kushiriki kombe la dunia katika ngazi mbalimbali ambapo wameanza mchakato wa kuifanyia maboresho ili kupiga hatua zaidi pale ambapo malengo hayakufikiwa.

Pia amewamwagia sifa mashabiki wa soka nchini akieleza kuwa wameliheshimisha taifa huko nje na kutengeneza taswira kubwa kuhusu soka la Tanzania kwa namna wanavyojitokeza uwanjani na kuujaza uwanja.

“Kama mnavyojua ligi zetu zinazochezwa na hata mashindano ya kimataifa bila mashabiki hakuna kitu, hawa wanatuheshimisha kimataifa kwa namna wanavyojitokeza uwanjani kuziunga mkono timu zao,” amesema.

NECTA yaonya udanganyifu mitihani kidato cha nne
Young Africans kuisubiri Singida Big Stars