Nahodha wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ amesema anafurahia kurudi uwanjani wakati timu yake bado ikiwa kwenye nafasi nzuri ya kutetea ubingwa wao wa Ligi Kuu.

Cannavaro hajaichezea Yanga tangu Oktoba mwaka jana kutokana na maumivu ya kisigino cha mguu aliyoyapata akiwa na timu yake ya taifa ya Zanzibar katika michuano ya Chalenji iliyofanyika Ethiopia.

Cannavaro  amesema amefurahishwa na bidii iliyokuwa ikioneshwa na wachezaji wenzake kwa kuipigania timu yao na kuifikisha hapo ilipo na anaamini wataendelea kufanya hivyo hadi mechi ya mwisho ili kutetea ubingwa wao msimu huu.

Beki huyo ambaye hivi karibuni alitangaza kujiuzulu kuichezea ‘Taifa Stars’, alisema hamasa aliyoikuta ndani ya timu inamfanya kufanya kazi ya ziada ili kurudi kwenye kikosi cha kwanza kama ilivyokuwa awali.

Alisema kitu hicho kimemfanya aongeze ari ya kufanya mazoezi ili aweze kurudi kwenye kiwango chake cha awali na kuanza kupangwa kwenye mechi za ligi ambazo zimekuwa na ushindani mkubwa.

Yanga inaongoza Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na pointi 46 sawa na Azam inayoshika nafasi ya pili, lakini Yanga ina uwiano mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.

Tumba Sued ‘Hatihati’ Jumamosi
Jerry Muro Amjibu Hadji Sunday Manara