Nahodha wa SSC Napoli, Giovanni di Lorenzo aliwatetea wachezaji wenzake baada ya kichapo cha mabao 3-0 kutoka kwa Inter Milan kwenye mechi ya Serie A.
Baada ya kichapo kizito nahodha huyo alisema: “Inatokea kwa wachezaji kupoteana mchezoni, ukiongozwa dhidi ya timu kubwa kama Inter Milan, ni ngumu sana kurudi mchezoni, lazima upambane hadi mwisho, bao la tatu lilituvuruga sana. Kuhusu ubingwa? Hapana, kwa sasa tunafikiria zaidi mechi zetu.
“Kila hatua tunaweza kufika mbali, Inter Milan ni nzuri sana kila mechi inapata matokeo mazuri, nimesikitishwa tumeshindwa kupata ushindi nyumbani.”
Mabao ya Inter Milan yaliwekwa kimiani na Hakan Calhanoglu katika dakika ya 44, Nico Barrela dakika ya 61 na Marcus Thuram (dk.85) ikiwadhalilisha mabingwa watetezi wa Serie A.
SSC Napoli imekuwa na msimu mbovu tofauti ilivyokuwa msimu uliopita ilipobeba ubingwa wa Serie A huku Mshambuliaji wa timu hiyo Victor Osimhen akiibuka mfungaji bora.
SSC Napoli imekumbana na kipigo hicho ikitokea kupasuka 4-2 dhidi ya Real Madrid katika mechi yao ya Kundi C ya Ligi ya Mabingwa Ulaya Jumatano iliyopita.
Wakati huo huo, kiungo wa AS Roma, Leandro Paredes amesema ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Sassuolo ulikuwani maalumu kwa ajili ya kocha wao Jose Mourinho.
AS Roma ilikuwa nyuma kwa bao 1-0 hata hivyo ikapambana na kuibuka na ushindi muhimu Serie A.
Akizungumza baada ya mechi Paredes alisema: “Mechi ilikuwa mkononi kwetu, kwa bahati mbaya tuliruhusu bao, lakini tukapambana tukapata ushindi, ushindi ulitusubiri, ilikuwa ushindi muhimu kwetu sio wa ajili yetu, hata kocha Jose Mourinho alipambana sana.”