Naibu Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua amesema ameridhishwa na oparesheni dhidi ya Pombe haramu, Mihadarati na Dawa za kulevya aliyoizindua mapema 2023, ambayo amedai imeanza kuzaa matunda kwani wengi wa wanawake wa Mlima Kenya wameshika ujauzito.
Gachagua aliyathibitisha hayo wakati wa maadhimisho ya Krismasi 2023, ambapo alikuwa amealika wakazi wa Mathira nyumbani kwake katika eneo la bunge hilo ili kula chakula pamoja.
Amesema, “juzi nimeita wazazi hapa, wakuje wachukue unga, mafuta…Walijaa hapa watu karibu 10, 000. Nikasema tupige laini ya kina mama ambao wako na watoto wadogo. Watoto walikuwa wanalia…Nilifurahi sana.”
“Haya, nikasema tena wale ambao wanangojea (akimaanisha wenye mimba) wapige laini, ingine hata mrefu zaidi (ilikuwa ndefu zaidi). Najivunia sana; ya kwamba jamii yetu imerudi. Tuna watoto ambao wanazaliwa. Tuna wanawake wajawazito, ambao wanatarajiwa kujifungua hivi karibuni ili jamii yetu iendelee kukua,” kauli ambayo iliwafanya watu kuangua vicheko.
Kabla kuwa mgombea mwenza wa Rais wa Kenya, William Ruto katika uchaguzi mkuu wa 2022 kupitia muungano wa Kenya Kwanza, Gachagua alihudumu kama mbunge wa Mathira kati ya 2017 hadi 2022 na kampeni hiyo imekuwa wakati Serikali ikipambana na Vita dhidi ya Dawa za kulevya na pombe haramu maarufu kama chang’aa.